Jumapili 4 Oktoba 2026 - 11:30
Swali Muhimu la Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf kwa Viongozi wa Iraq

Hawza/ Sayyid Sadruddin al-Qabanji, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu, aliwauliza viongozi wa Iraq: Je, inajuzu kwa Iraq kushiriki katika mzingiro wa kidhulma dhidi ya nchi jirani, rafiki na nchi ambayo ilisimama pamoja nasi katika siku za shida?

Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin al-Qabanji, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husseiniya Kuu ya Fatimiyya, Najaf Tukufu, alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani, ya kikanda na ya kimataifa.

Pongezi kwa Siku ya Mamlaka ya Nchi ya Iraq na Kuondoka Vikosi vya Muungano

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu alianza hotuba yake kwa kusema: Tunawapongeza wananchi wote na vikosi vyetu vya usalama kwa ushindi huu wa kuondoka kwa vikosi vya muungano tarehe 30 Septemba, baada ya miaka 23 ya mapambano katika ngazi zote za kisiasa, kijeshi na kiusalama.

Alieleza tukio hili kuwa ni “hatua kuelekea kufikiwa kwa mamlaka kamili ya kitaifa”, na kuongeza: Kuna hatua nyingine zinazohitajika pia, miongoni mwa hizo ni suala la mapato ya mafuta ya Iraq; mapato hayo yanapaswa kuwa mali ya Iraq yenyewe na kupokelewa moja kwa moja kutoka katika nchi ambazo Iraq inaziuza mafuta, wakati kwa sasa mapato hayo yanawekwa katika Benki Kuu ya Marekani.

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu, akirejea taarifa ya wizara husika iliyotolewa jana kwamba imepokea kiasi fulani cha dola kutoka Marekani, alisema: Hili ni jambo la kufungua njia; hizi ni fedha zilezile za Iraq ambazo zimekuwa zikishikiliwa na Marekani, na jambo hili lina maana kwamba Iraq bado inaishi chini ya mamlaka isiyokamilika.

Mzingiro wa Safari za Ndege za Iran; Iraq Inawezaje Kushiriki katika Dhulma Hii?

Katika sehemu inayohusu masuala ya kikanda, Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Qabanji aliuliza: Je, inajuzu kwa Iraq kushiriki katika mzingiro huu wa kidhulma dhidi ya nchi jirani, rafiki na nchi ambayo ilisimama pamoja nasi katika siku za shida? Alibainisha kwamba nchi nyingine kama China, Armenia, Malaysia, Vietnam, Pakistan, Russia na Uturuki hazijakubali marufuku hii.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu, akiuliza ni kwa namna gani Iraq inaweza kuwa mshirika katika dhulma hii, alitoa wito wa “kuupitia upya uamuzi huu”, na kutangaza: Tunasimama pamoja na wananchi wa Iraq ambao wamejitokeza mitaani kulaani mzingiro huu na kudai uondolewe, na tunawaunga mkono.

Kukamilishwa kwa Baraza la Mawaziri; Utawala wa Marekani Wazuia Kuundwa Wizara za Ulinzi na Mambo ya Ndani

Kuhusu masuala ya ndani, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu alisema: Katika suala la kukamilishwa Baraza la Mawaziri, bado kuna wizara muhimu kama Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi ambazo ziko wazi bila mawaziri kutokana na kuingiliwa na utawala wa Marekani; jambo hili lina maana kwamba Iraq bado iko chini ya utawala wa kigeni, na hili ni jambo linalokataliwa na linapingana na mamlaka ya kitaifa iliyotangazwa. Mradi wa mamlaka ya kitaifa ni mradi mkubwa na ni ushindi wa wananchi wa Iraq, lakini unahitaji kukamilishwa kwa vipengele vingine vya mamlaka hiyo.

Khutba ya Kidini: Uwiano kati ya Akili na Matamanio

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Tukufu, katika khutba yake ya kidini, baada ya kutoa nasaha kuhusu kumcha Mwenyezi Mungu, alizungumzia suala la kuweka uwiano kati ya akili na matamanio, na akatoa dalili kwa aya hii:

﴿فَأَمَّا مَنْ طَغَیٰ وَآثَرَ الْحَیَاةَ الدُّنْیَا فَإِنَّ الْجَحِیمَ هِیَ الْمَأْوَیٰ ۝ وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَی النَّفْسَ عَنِ الْهَوَیٰ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِیَ الْمَأْوَیٰ﴾

“Ama yule anayevuka mipaka na akachagua maisha ya dunia, basi hakika Jahannamu ndiyo makazi yake. Na ama yule anayehofia kusimama mbele ya Mola wake na akaizuia nafsi yake kufuata matamanio, basi hakika Pepo ndiyo makazi yake.”

Alinukuu riwaya kutoka kwa Imam Swadiq (as), katika kujibu swali la iwapo Malaika ni bora kuliko wanadamu, ambapo alisema kwamba Imam Ali (as) amesema:

«إن الله رکّب فی الملائکة عقلاً بلا شهوة، ورکّب فی البهائم شهوة بلا عقل، ورکّب فی بنی آدم کلتیهما، فمن غلب عقله شهوته فهو خیر من الملائکة، ومن غلبت شهوته عقله فهو شرّ من البهائم»

“Hakika Mwenyezi Mungu ameweka ndani ya Malaika akili bila matamanio, na ameweka ndani ya wanyama matamanio bila akili, na kwa wanadamu ameweka vyote viwili. Basi yule ambaye akili yake itayashinda matamanio yake ni bora kuliko Malaika, na yule ambaye matamanio yake yataishinda akili yake ni mbaya zaidi kuliko wanyama.”

Mwanadamu Atakuwaje Miongoni mwa Watu wa Peponi?

Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Qabanji, alipouliza swali: “Mwanadamu atakuwaje miongoni mwa watu wa Peponi?”, alirejea riwaya kutoka kwa Mtume (saww) na Imam Jawad (as).

Katika mojawapo ya riwaya hizo, Mtume (saww) alimpa mwongozo wa kiroho mtu aliyekuwa akitaka kujua njia ya kuingia Peponi. Aidha, katika riwaya kutoka kwa Imam Jawad (as), imesisitizwa kusoma aya maalumu, kama vile Sura Tukufu ya Insan/“Inzalna”, pamoja na kuendelea kufanya istighfari.

Kuuwawa kiShahidi kwa Kumayl bin Ziyad al-Nakha’i

Pia alirejea tukio muhimu la kihistoria, yaani kuuwawa kishahidi Swahaba mtukufu Kumayl bin Ziyad al-Nakha’i katika mwaka wa 82 Hijria, tarehe 21 Rabiul-Thani.

Imenukuliwa kwamba Hajjaj al-Thaqafi, ambaye wakati wa Marwan alikuwa gavana wa Iraq, alikuwa akimtafuta Kumayl bin Ziyad, lakini Kumayl alimkimbia. Hajjaj alimtaka tena Kumayl, lakini Kumayl akajificha ili asifikike kwake. Kufuatia tukio hilo, Hajjaj alikataa kulipa mishahara ya watu wa kabila la Kumayl, yaani akaiwekea “kabila la Kumayl mzingiro wa kiuchumi.”

Kumayl alipogundua hali hiyo, alisema: “Mimi ni mzee ambaye umri wangu umefikia mwisho, na haifai kuwa watu wangu wanyimwe haki zao.” Kwa sababu hiyo, alijisalimisha kwa Hajjaj ili mzingiro huo uondolewe kwa watu wake.

Hajjaj alipoamuru akatwe kichwa, Kumayl alimwambia Hajjaj: “Amirul-Muuminina Ali (as) aliniambia kwamba wewe ndiye utakayeniua.” Kisha Hajjaj akakata shingo yake.

Pia alirejea tukio jingine la kihistoria ambapo, kwa mujibu wa yaliyoandikwa katika vitabu vya historia, miongoni mwao Tārikh al-Tabari, kwa amri ya Ziyad bin Abihi katika mwaka wa 51 Hijria, watu 50,000 kutoka Kufa na Basra walihamishwa kwenda Khurasan; watu 25,000 kutoka Kufa na 25,000 kutoka Basra.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha